Kila inapofika wakati wa taarifa za habari huwa ninaanza
kutafakari kuwa leo televisheni zetu zitatuonesha picha za namna gani. Huu ni
wakati ambapo hua natafuta remote control na kukaa nayo karibu, wengi mnaweza
msinielewe kwanini nafanya hivyo, hua nafanya hivyo ili kuweza kuwa na wasaha
wa kubadilisha stesheni pindi zinapooeneshwa picha zisizofaa.
Kwanini ninaziita picha zisizofaa kuoeneshwa, kwa sababu ni
picha zinazobadilisha hisia za mwili na kuufanya mwili kutoa vichocheo vya
mwili ambavyo huubadilisha hisia za mwili kabisa. Picha zinaoenesha maiti
zisizofunikwa na huku zikwa zilizoharibika vibaya iwe ni ajali au vinginevyo,
picha za watu wenye magonjwa ya ngozi ambayo yamewaharibu sana, picha za watu
waliokatwa viungo, na picha nyingine nyingi ambazo hazifai hata kuzitazama kama
haujajianda kufanya hivyo.
mwanadamu ameumbwa kwa namna ya pekee sana, milango yake mitano
ya mfumo wa fahamu humpa ishara ya matukio mbalimbali yanayotokea kwenye
mazingira yanayomzunguka kwa jinsi hii mwanadamu amepewa uwezo wa kustahimili
kuishi kwenye hii dunia yenye ushindani, bila ya kuwa na milango hii ya fahamu
mwanadamu asingeweza kuona, kuhisi kwa kugusa, kusikia, kunusa harufu na kupata ladha mbalimbali kwa kutumia ulimi.
Mwili hupokea viashiria vya utambuzi na fahamu kwa namna tofauti kutegemea
aina ya kiashiria na pia husaidia kuweka
kumbukumbu kwenye ubongo wa binadamu. Hivyo basi waandishi wa habari kuweni
makini sana na taarifa zenu na hasa picha mkijua ya kua picha hizo zinamchango
mkubwa sana kwenye maisha ya binadamu.
Karibu taarifa za
siku za vituo vya habari hapa nchini hua ni kuanzia saa moja jioni hadi saa
tatu usiku, huu ni muda ambao watoto wamesharudi kutoka shuleni na watu wazima
wamerudi kutoka kwenye mihangaiko yao ya kila siku, huu ni muda ambao familia
nyingi hukaa pamoja kupumzika huku wakipata riziki yao ya jioni na wakiti
huohuo wakiangalia taarifa za habari, hivyo kufanya taarifa za habari
kuangaliwa na marika yote, kwa watoto hizi ni picha ambazo huwaharibu
kisaikolojia na wakati mwingine huwajengea uoga ndani yao. Na si watoto tu hata
watu wazima hushindwa hata kupata usingizi kutokana na picha ambazo wameziona
kwenye televisheni. Wazazi wengi siku hizi wameshaanza kuwazuia watoto wao
wasingalie baadhi ya vipindi basi sasa isifike wakati mkawalizimisha wazazi
kuwazuia watoto wao kuangalia hata taarifa za habari.
Je? mshawahi
kufikiria au kuchunguza ni watu wangapi hushindwa kuangalia maati kwenye
matukio ya kuaga miili ya marehemu
kwenye misiba ya kawaida tu inayotokea mitaani kwetu? Sio kwamba hawapendi ila
wameumbwa kutokuweza kuhimili matukio kama yale, je kwanini waandishi wahabari
mnawalizimisha watanzania hawa kuangalia picha za namna hii bila ridhaa yao.
Sasa na kibaya zaidi kinachosikitisha ni kwamba mara nyingi wanashindwa hata
kutoa tahadhari juu ya picha watakazozionesha sanasana wanaomba samahani wakati
tayari picha zimeshaoneshwa.
Kwakweli inasikitisha sana kuona kuwa vyombo hivi vya habari
hutoa picha hizi bila hata ya kuzihariri (editing) na kuficha sehemu zile
zinazoonekana kuwa hazistahili kuonenshwa kwenye jamii ya watu wengi.
Tumeshawahi kujiuliza kuwa kwanini vyombo vya habari vikubwa vya nchi za nje
havioneshi picha kama hizi zinazoeneshwa na televisheni za hapa nyumbani?
Mfano mdogo sana na wa kuigwa ni huu hapa, Kwa wale
mashibiki wa mpira mnaopenda kuangalia ligi za mpira hasa uingreza mtakubaliana
na mimi, pindi mchezaji anapopata dhahama la kuumia vibaya kiasi cha kuvunjika
vibaya au kupoteza fahamu iwe ni kwa kuchezewa vibaya au vinginevyo, matukio
yale huwa hayaoneshwi kabisa na wala sehemu ya kiungo cha mwili cha mchezaji
kilichoumizwa vibaya hakitoeneshwa. Moja ya sababu chache za kufanya hivyo ni,
wanazingatia utu, na heshima ya mchezaji, pia wanajua kuwa kuna watoto wengi
wenye ndoto za kuwa wachezaji mpira pindi watakapona picha kama hizi wanaweza
kupata woga na kuamua kuachana na ndoto hizo, je? Vipi watoto wa watanzania
wenye ndoto za kuwa madaktari mnapowaonesha picha za magonjwa ya kutisha,
mnafikiri mnajenga nini vichwani mwao?
Utu wa mwanadamu ni muhimu sana ukalindwa, je kwanini
waandishi wa habari mnashindwa kulinda utu wa wagonjwa na hata maiti za ndugu
zetu waliopoteza maisha yao. kama ni wewe mwandishi umepata ugonjwa wa ngozi
ambao umetokea kukuharibu kabisa sehemu
za uso , Je utakua tayari picha zako zikaoneshwa Tanzania nzima?
Acheni jamani udhalilishaji wa huu, kama kuna mtu anatatizo
na mnataka kuwashirikisha watanzania juu ya tatizo lake, kwa mfano ugonjwa, kwa
nia ya kutaka kumsaidia kupata msaada kutoka kwa watanzania wenzake, basi
msichukue wasaha huo kumdhalilisha kwa kuwaonesha watanzania wote picha za
ugonjwa aliokua nao, masikini kwa kuwa watanzania
hawa ni wanyonge kwa umasikini hawana budi kukubali kuoneshwa ili wapate
msaada, hapana sio sawa kabisa.
Ndugu zangu waandishi muwe makini sana na hizi picha
mnazozionesha kwenye vituo vyenu vya televisheni, muwe na uhakika zitaleta
mwonekano wa namna gani katika jamii mnayowaonesha, jiulizeni maudhui ya
kuonesha picha za namna hiyo, jiulizeni faida na hasara na kasha jiulizeni je
ni muhimu sana mkazionesha? Na kama ni muhimu kuonekana basi je? zionekane katika mwonekano wa namna gani? heshimuni utu wa watu, wafunikine wagonjwa,
zifunikeni maiti na ziharirini picha kabla hamjazionesha na ondoeni sehemu
zisizofaa kuoneshwa kwenye jamii ya watanzania ili kujenga Tanzania yenye
kuheshimu na kuthamini watu wake.